Mwanachama na mfadhili wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji “Mo”, amesema nia yake ni kuifanyia makubwa klabu hiyo, siyo tu Tanzania bali Afrika kwa jumla.

“Mo” alisema hayo alipokuwa akihojiwa wakati wa Tamasha la Simba Day lililofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa ambapo Simba ilicheza mechi dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda na kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Akizungumza kabla ya mchezo huo kuanza, “Mo” alisema anafarijika kuona Simba ina mipango mizuri, akiwa mmoja wa wanachama wa klabu hiyo nia yake ni kuona Simba inafanya vizuri kimataifa na siyo kuishia ndani ya Tanzania pekee.

“Ni kweli nimekuwa nikijitolea ndani ya Simba, sisi Wanasimba tunapenda kuona timu yetu ikifanya vizuri kuanzia ligi za ndani hadi nje, ndiyo maana unaona hata usajili umekuwa ni wa wachezaji wazoefu.”

“Nia yangu kubwa ni kuiona Simba ikiwa bingwa wa Afrika”.  Alisema “Mo”

Mfadhili huyo wa klabu ya Simba amekua katika harakati ya kutaka kuimiliki klabu hiyo kwa mfumo wa hisa, na sasa anasubiri ridhaa ya wanachama ambao watakutana katika mkutano mkuu August 13, ambapo moja ya ajenda katika mkutano huo ni kupitisha mabadiliko ya katiba yatayoendana na mfumo mpya.

Wachezesha kamali wabanwa, sasa kuanza kulipa kodi TRA
Mbaraka Yusuph Achimba Mkwara Mzito Ligi Kuu Bara