Hatimae sokomoko la beki wa kulia wa klabu ya Simba Mohamed Hussein Tshabalala, limemalizwa rasmi hii leo, baada ya viongozi wa klabu hiyo kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Meneja wa mchezaji huyo Henry Mzozo, amefanya mahojiano maalum na Dar2 na kueleza taratibu zilizochukuliwa na viongozi wa Simba hadi kufikia hatua ya kukamilisha suala la kusainiwa kwa mkataba mpya wa Tshabalala.

Mzozo amesema umakini na maelewano mazuri baina pande hizo mbili vimekua chachu ya kukamilisha mchakato wa mchezaji wake kuendelea kutambuliwa kama mchezaji halali wa Simba SC.

“Ninaweza kusema Tshabalala amebakisha kama asilimi 20, kukamilisha taratibu zote za kuendelea kuitumikia simba, labda nikuweke wazi kinachoendelea hivi sasa ni masuala ya kibenki ambayo yanakamilisha huu mchakato,

“Viongozi wa Simba walikua na mazungumzo ya muda mrefu na Tshabalala na nikueleze kwamba, hatua hii ilianza tangu mwanzoni mwa msimu huu, na ukaribu uliopo baina ya mchezaji wangu na uongozi wake ndio imekua chachu ya mafanikio ya kusainiwa kwa mkataba wa miaka miwili” Alisema Mzozo

Hata hivyo Mzozo amekanusha taarifa za kuwepo kwa ushawishi ambao unadaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa Young Africans wa kumsajili Mohamed Hussein katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

“Ninaweza kusema katika suala hili Yanga walizushiwa, lakini hakuna ukweli wowote kuhusu mipango iliyokua ikiendelea chini chini kumuhusu Tshabalala, japo kwa upande wangu ninazichukulia taarifa hizo kama kunogesha mchezo wa soka ambao siku zote umekua na maneno mengi.” Aliongeza Mzozo.

Mohamed Hussein alikua amesaliwa mkataba wa miezi minane wa kuitumikia klabu ya Simba, na hatua iliyofikiwa ya kusainiwa mkataba mpya, inamuwezesha mchezaji huyo kuendelea na maisha ya Msimbazi hadi mwaka 2018.

Liverpool, Celtic, Newcastle Utd Zamuwania Steven Gerrard
Rais Magufuli asaini Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016