Jopo la madaktari wa timu ya taifa ya Misri, limeendelea kuwa njia panda kuhusu mustakabali wa mshambuliaji Mohamed Salah kama ataweza kucheza mchezo wa kwanza wa kundi A wa fainali za kombe la dunia, dhidi ya Uruguay siku ya ijumaa.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, alipatwa na jeraha ya bega la mkono wake wa kushoto wakati wa mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya kati ya Liverpool na Real Madrid, baada ya kuangushwa na Sergio Ramos, Mei 26.

Kwa mara ya kwanza Salah alionekana akifanya mazoezi na wachezaji wenzake jana jumatatu, lakini jopo la madaktari limeshindwa kutoa taarifa za uhakika kama mshambuliaji huyo amepona na ataweza kucheza dhidi ya Uruguay.

Mtendaji mkuu wa timu ya taifa ya Misri Ehab Lehita, amesema bado wanaendelea kufuatilia hali ya Salah, lakini ni mapema mno kusema kama atakua tayari kucheza siku ya ijumaa.

“Tunaendelea kumfuatilia kwa ukaribu ili kujiridhisha kama yupo FIT kwa asilimi 100, lakini ni mapema sana kuthibitisha kama ataweza kutumika kwenye mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi ambao tutacheza dhidi ya Uruguay siku ya ijumaa.” Alisema kiongozi huyo

“Jeraha lake kwa kifupi linaendelea vizuri tangu alipofanyiwa matibabu nchini Hispania, madaktari wanafuatilia hali yake kila kukicha na ndio maana mmemuona akifanya mazoezi na wenzake.”

“Kila siku hupatiwa matibabu kama ilivyoagizwa na waliomfanyia tiba akiwa Hispania, tunaamini tunafuata masharti tulioagizwa, na tuna imani atacheza soka tena kwa siku za karibuni, japo hatuwezi kutambua kama atakua sehemu ya kikosi siku ya ijumaa.”

Endapo Salah atashindwa kucheza mchezo dhidi ya Uruguay, matarajio yake makubwa ni kucheza mchezo wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya wenyeji Urusi Juni 19, kabla ya mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ambapo Misri watapapatuana nan Saudi Arabia mjini Volgograd siku sita baadae.

Tayari kikosi cha misri kimeshawasili nchini Urusi, kwa ajili ya maandalizi ya mwisho, kabla ya kuanza mchaka mchaka wa kusaka ubingwa wa dunia kwa mwaka huu 2018.

Kamati yaundwa kuchunguza mwanamke aliyejifungua mikononi mwa polisi
Serikali yaziweka mtegoni kampuni za ununuzi wa Pamba