Meneja wa klabu ya Liverpool Juergen Klopp amepongeza uwezo wa mshambuliaji wa klabu hiyo Mohamed Salah, baada ya kurejea kikosini na kufunga bao kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa soka nchini England Man City.

Salah aliifungia Liverpool bao la kwanza dakika ya 63, baada ya  mshambuliaji wa pembeni wa Man City Leroy Sane kufunga bao la kuongoza  dakika ya 57 na baadae Sadio Mane kufunga bao la ushindi kwa majogoo wa jiji kwa mkwaju wa penati dakika ya 90.

Mchezo huo ulikua wa kwanza kwa mshambuliaji huyo kutoka nchini Misri, tangu alipojiunga na kambi ya maandalizi ya kikosi cha Liverpool huko nchini Marekani.

“Ameonyesha anaweza kutimiza majukumu yake wakati wowote, ni hatua nzuri kwake na kwa klabu katika harakati za kujiandaa na msimu mpya wa ligi ambao tunaamini utakua na kila aina ya upinzani kutokana na maandalizi yanayoendelea kwa timu shiriki,” Alisema Klopp alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo uliounguruma majira ya leo alfajiri.

Liverpool watacheza mchezo mwingine wa kirafiki kupitia michuano ya kombe la mabingwa (Champions Cup) siku ya jumamosi dhidi ya wapinzani wao kutoka England Manchester United.

CBF, Tite wasaini mkataba hadi 2022
Afariki akiwa mikononi mwa Polisi

Comments

comments