Ndoto za mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Mohamed Salah za kucheza fainali za kombe la dunia kwa mara ya kwanza huenda zikayeyuka, kufuatia majeraha aliyoyapata wakati wa mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid usiku wa kuamkia leo mjini Kiev, Ukraine.

Salah alilazimika kutolewa nje ya uwanja na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Lallana kipindi cha cha kwanza, baada ya kuumia bega la mkono wake wa kushoto.

Mshambuliaji huyo alipatwa na maswahibu hayo, baada ya kuangushwa chini na mlinzi wa Real Madrid Sergio Ramos, walipokua kwenye harakati za kuuwania mpira uliokua unakwenda langoni ma mabingwa mara tatu barani Ulaya (The Galacticos).

Meneja wa Liverpool Jürgen Klopp alithibitishja katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo uliomalizika kwa Liverpool kufungwa mabao matatu kwa moja, na kueleza maendeleo ya hali ya Salah, aliyetoka uwanjani dakika ya 30.

“Ameumia sana, lakini siwezi kusema kama ataweza kupona leo ama kesho, kwa sababu vipimo havijafanyika, ila kwa taarifa za awali kutoka kwa daktari wa timu yetu, ameniambia Salah ameumia sana katika bega lake,” Alisema Klopp alipozungumza na waandishi wa habari.

“Kimtazamo huenda ikamchukua muda mrefu kupona, lakini tusubiri vipimo vitakua na majibu sahihi ya kueleza ni muda gani atakua nje ya uwanja.

“Sikupendezwa na alichofanyiwa Salah, kwa sababu lilionekana kama shambulio la makusudi alilofanyiwa, Ramos alistahili kuadhibiwa kwa alichomfanyia mchezaji wangu, lakini kwa mshangao mkubwa aliachwa na mwamuzi.” Aliongeza Klopp.

Mohamed Salah tayari ameshatajwa kwenye kikosi cha Misri kitakachoshiriki fainali za kombe la dunia kuanzia Juni 14 nchini Urusi, lakini bado upande wa madaktari wa timu hiyo ya taifa kutoka Afrika, hawajasema lolote kuhusu uwezekano wa mshambuliaji huyo kucheza fainali hizo ama la.

Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Mei 28, 2018
Video: Jinsi Bale alivyosherekea ushindi na mashabiki Madrid