Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Mohamed Salah atajiunga rasmi na timu ya taifa ya Misri majuma matatu yajayo, kwa ajili ya mshike mshike wa kombe la dunia ambao unatarajia kuanza Juni 14 nchini Urusi.

Shirikisho la soka nchini Misri limethibitisha taarifa za mshambuliaji huyo, baada ya kufanyiwa matibabu akiwa mjini Valencia, Hispania.

Salah aliumia bega la mkono wake wa kulia mwishoni mwa juma lililopita, akiwa katika mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid ambao waliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja.

Mshambuliaji huyo aliwasili mjini Valencia juzi jumanne kwa matibabu, chini ya usimamizi wa daktari wa timu ya taifa ya Misri.

Shirikisho la soka nchini Misri limeeleza kuwa, Salah atakua fit ndani ya muda huo na atacheza katika fainali za kombe la dunia.

Misri wataanza kibarua cha kusaka ubingwa wa kombe la dunia kwa kucheza dhidi ya Uruguay Juni 15, na kimahesabu ya muda, Salah hatoweza kuwa sehemu ya kikosi cha siku hiyo.

Salah anatarajiwa kuanza kuitumikia Misri katika mchezo wa pili hatua ya makundi Juni 19, ambapo Misri watapambana na wenyeji Urusi mjini Saint Petersburg.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 31, 2018
Video: Mazishi ya Bilago yaibua utata, Bashiru azua gumzo ndani na nje ya CCM

Comments

comments