Katibu mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohammed Kiganja amewataka walimu wa shule za msingi nchini, wanaoandaa timu kwa ajili ya mashindano ya Umitashumta kuepuka kuwatumia wachezaji mamluki katika mashindano hayo ambayo yanaendelea nchi nzima katika ngazi mbalimbali.

Kiganja aliyasema hayo juzi alipoitembelea kambi ya mazoezi ya timu ya Umitashumta ya Manispaa ya Kinondoni katika shule ya Sekondari ya Lord Baden iliyoko Bagamoyo mkoani Pwani.

Alisema, kuwatumia mamluki katika mashindano hayo ni kuyaondolea hadhi na kuwanyima haki walengwa hali ambayo alisema ni makosa kisheria na kwamba, yeyote atakaethubutu kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

“Mashindano haya ni kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi, naomba washirikishwe hao tu, kamwe msijaribu wala kuthubutu kuwatumia mamluki katika mashindano hayo, sioni mantiki ya kufanya hivyo, waandaeni wanafunzi wenu kwa ushindani itakuwa vizuri kuliko kutumia mamluki ili kupata ushindi wa hila, akibainika mwalimu ametumia mamluki katika timu yake, ngazi husika za maamzi zimchukulie hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na timu yake kufutwa na kuondolewa mashindano” alisema Kiganja.

Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni Kiduma Mageni mbali na kumshukuru Kiganja alimhakikishia kuwa, timu yake haitakuwa na mchezaji mamluki hata mmoja, haijawahi na haitatokea na kuunga mkono kuchukua hatua dhidi ya watakaobainika kuwatumia wachezaji mamluki.

Aidha mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano Umitashumta Manispaa ya Kinondoni, Masau Bwire alisema, katika mashindano ya Mkoa wa Dar es salaam yanayoanza Ijumaa hii, Juni 10, 2016  katika viwanja vya Chuo Kikuu, Mlimani yakishirikisha timu za Manispaa ya Kinondoni, Ilala na Temeke hawatarajii kuwepo kwa vitendo vya kihuni kwa timu kuchezesha wachezaji mamluki na ikitokea, walimu waliohusika ni majipu tayari, lazima watumbuliwe!

Video: COTWU wampongeza Rais Magufuli, Wazungumzia hali ya Chama
Bonta aeleza sababu ya Mwalimu Nyerere kukataa kukutana na Muhammad Ali