Kiungo mshambuliaji wa Young Africans, Bernard Morrison ameishtaki klabu hiyo TFF, akidai kutotambua mkataba mpya wa miaka miwili unaodaiwa kuwa alisaini kwa makubaliano maalum.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya mwenyekiti wake, Elias Mwanjala, jana Jumatano ilianza kusikiliza kesi hiyo katika viunga vya Shirikisho hilo.

Mwanjala amesema mchezaji huyo amewasilisha ushahidi wake katika kesi hiyo ambayo uamuzi unaweza kutolewa leo Alkhamis, kutegemeana na usikilizaji wa pande zote, mashahidi na kamati kuridhishwa na ushahidi utakaowasillishwa.

Amesema Morrison amefungua kesi hiyo mwenyewe na alifika kwa ajili ya utetezi wa hoja zake huku Young Africans ikiwakilishwa na viongozi mbalimbali akiwemo mwanasheria ambaye pia ni kaimu katibu mkuu, Simon Patrick na makamu mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela.

“Sisi kazi yetu ni kusikiliza na kupitia ushahidi ambao pande zote mbili umewasilisha kwetu. Kama hautoshi, basi tutawapa muda zaidi, lakini kama tumeridhishwa tutatoa uamuzi, lakini siyo leo (jana) kwani kuna malalamiko mengi ukiachana na hayo,” amesema Mwanjala.

Amesema kuwa mbali ya kesi hiyo, kamati yake pia inasililiza malalamiko yaliyowasilishwa na Young Africans dhidi ya Simba ikiituhumu kufanya mazungumzo na Morrison kinyume na utaratibu, ikidai amekuwa akishawishiwa na mabingwa hao ajiunge nao.

Klopp aahidi kutetea taji 2020/21
Sheria za wanawake na watoto zatakiwa kutafsiriwa