Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri ametangaza dhamira ya kufikisha mabao 20 msimu huu wa 2022/23, ambao umepangwa kufikia kikomo mwezi Mei 2023.

Phiri aliifungia Simba SC mabao mawili kati ya matatu yaliyoipa ushindi klabu hiyo ya Msimbazi Jumamosi (Desemba 03) dhidi ya Coastal Union iliyocheza nyumbani Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Zanaco FC ya nchini kwao Zambia, amesema amedhamiria kufunga mabao 20, katika msimu wake wa kwanza akicheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara, na ikiwezekana kuwa mfungaji Bora wa msimu.

Amesema kama Mshambuliaji atahakikisha anaipambania Simba SC na kisha kufikia malengo aliyojiwekea hadi mwishoni mwa msimu huu, na ikitokea anashindwa kuyafikia hatojihisi furaha kabisa.

“Sitakua na furaha kama nisipofikisha mabao 20 ukiwa ni msimu wangu wa kwanza ndani ya Simba SC, malengo yangu ni kufunga mabao hayo, ninaamini nitafanikiwa kwa kushirikiana na wenzangu.”

“Hivyo basi nina kibarua kigumu cha kufikisha idadi hiyo ya mabao, kikubwa nitakachokifanya ni kutimiza malengo ya timu na yangu binafsi niliojiwekea.”

“Nikiwa kama Mshambuliaji nitahakikisha ninatumia vema kila nafasi nitakayoipata kufunga mabao pia kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzangu.” Amesema Moses Phiri

Hadi sasa Moses Phiri ameshaifungia Simba SC mabao 10 katika Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akionyesha kuwa na ushirikiano mkubwa na Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chota Chama.

ICC yapinga kuundwa Mahakama ya uhalifu wa Ukraine
Maporomoko yasababisha vifo watu 27