Moto uliozuka kwenye msitu katika jimbo la California nchini Marekani umesababisha vifo vya watu 25, kwa mujibu wa maafisa wa Serikali.

Idadi hiyo imeripotiwa baada ya kubainika kwa miili 14 karibu na mji wa Paradise Kusini mwa jimbo hilo, na kufanya idadi ya waliothibitishwa kupoteza maisha kufikia 25. Watu wengi zaidi kati ya hao wameripotiwa kufariki karibu na Malibu.

Aidha, inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 250,000 walilazimika kukimbia makazi yao wakiepuka moto mkubwa uliozuka katika jimbo hilo.

Rais Donald Trump, ameeleza kuwa kuzuka kwa moto huo kumetokana na usimamizi mbovu wa misitu katika eneo hilo, licha ya kuwa Serikali imekuwa ikitoa pesa nyingi kwa ajili ya usimamizi.

“Hakuna sababu yoyote ya moto huu mkubwa katika misitu ndani ya California isipokuwa usimamizi mbovu wa misitu”, Rais Trump aliandika Twitter.

Kwa mujibu wa BBC, moto huo ulianza kusambaa kupitia Kaunti ya Butte, Alhamisi ya wiki hii. Kikosi cha zima moto hakikuwa na uwezo wa kutosha kuzuia uharibifu uliotokea kwenye mji wa Paradise.

Moto mwingine ulizuka Ijumaa, kusini mwa ufukwe wa Malibu na hivi sasa umeripotiwa kuongezeka mara dufu.

Vikosi vya kuzima moto vimeeleza kuwa kuna matumaini ya kutumia uelekeo mpya wa upepo kujaribu kuzima moto huo.

Jana, moto huo uliripotiwa kuharibu hekari 100,000. Mkuu wa kitengo cha zima moto alieleza kuwa inaweza kuchukua hadi wiki tatu kuweza kudhibiti kikamilifu moto huo.

NECTA yatangaza tarehe ya kuanza mitihani kidato cha pili
Wananchi wajitolea kujenga Kivuko