Watoto wachanga pamoja na mama wazazi na wajawazito wamenusurika kifo baada ya moto kuzuka jana usiku katika wodi ya wazazi ya hospitali ya Mbagathi jijini Nairobi nchini Kenya.

Baadhi ya wanawake wajawazito walilazimika kukimbia usiku na kutumia muda wa usiku wakiwa kwenye baridi kali wakati wafanyakazi wa hospitali hiyo walipokuwa wanaendelea kufanya juhudi za kuuzima moto huo.

“Watoto 16 waliokuwa wamezaliwa jana walikuwa katika sehemu maalum ya kuhifadhia watoto wachanga lakini kwa bahati nzuri hakuna mtoto aliyepoteza maisha,” alisema Michael Muchiri, mkuu wa jeshi la polisi wa eneo la Kilimani.

Kwa mujibu wa Muchiri, Vichanga hao walihamishiwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH) na wako katika hali nzuri kiafya.

Hivi karibuni, hospitali ya Mbagathi ilizua gumzo kwenye vyombo vya habari kuhusu kuwa na miundombinu mibovu hasa katika wodi ya wazazi.

Ripoti iliyotolewa kwenye vyombo vya habari ilionesha kuwa ingawa hospitali hiyo ilitumia sh. 220 milioni za Kenya miaka minne iliyopita kwa ajili ya ukarabati, tayari nyufa zimeonekana kwenye paa na kuta za wodi hiyo.

Mapema leo, Umoja wa Wauguzi wa Kenya (KNUN) ulikosoa vikali menejimenti ya hospitali hiyo kwa kutochukua hatua stahiki baada ya kupewa tahadhari na wahandisi waliokagua jengo la hospitali hiyo.

*Picha iliyotumika imechukuliwa kwenye mtandao wa VOA, siyo ya tukio husika.

Qchillah asitisha kuacha muziki, adai haikuwa kiki
TFDA yawasaka wanaotangaza dawa za kuongeza maumbile

Comments

comments