Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA) limemfungulia rasmi mashtaka meneja wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho kuhusu matamko yake wakati wa mchezo kati ya timu hiyo na Newcastle United ulioshuhudiwa Oktoba 6 mwaka huu.

Katika maelezo ya mashtaka hayo, kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 anadaiwa kutumia maneno ya matusi na lugha isiyofaa muda mfupi baada ya Man Utd kupata ushindi wa 3-2 na kuondoa ukame wa ushindi uliokuwa unawatafuna.

FA imempa Mourinho muda wa hadi Oktoba 19 mwaka huu, saa kumi na mbili kamili kwa saa za eneo hilo awe amejibu mashtaka hayo dhidi yake.

Hili ni pigo lingine la presha kwa Mourinho ambaye amekuwa akiwekwa kitimoto cha kutimuliwa kutokana na muenendo wa matokeo yasiyoridhisha ya timu yake.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu, Man Utd ilifanya maajabu ikitumia dakika 20 za kipindi cha pili kupachika magoli matatu wakiwaacha nyuma Newcastle walioongoza kwa magoli mawili tangu kipindi cha kwanza.

Juan Mata, Anthony Martial na Alexis Sanchez ndio walioipa Man United kiburi cha ushindi katika mechi hiyo.

Basi la New Force lapata ajali Mlima Kitonga
Video: Lema afunguka kuhusu 'Mo Dewji' ataka wachunguzi wa Kimataifa