Meneja wa Manchester United, José Mourinho ametamba na kupuuzia maneno ya waliokuwa wanamshambulia awali, baada ya timu yake kuichapa Bournemouth 2-1 leo jioni.

Mourinho amefunguka baada ya mchezo huo na kueleza kuwa hajali mitazamo ya watu kuhusu kuanza vibaya kwa timu hiyo kwani msamiati huo hauelewi na kuwataka wanaoutumia kutomzeesha.

“Sielewi! Timu yangu iliniambia mwanzo wetu ulikuwa ni kitu bora zaidi ambacho tumewahi kuwa nacho. Ninapenda wimbo wa ‘Shambulia! Shambulia! Shambulia! [unaoimbwa na mashabiki] lakini pia tunahitaji kuwa na ngome nzuri ya ulinzi. Hakika sielewi mitazamo hiyo ambayo inaniongezea mvi kichwani kwangu,” alisema.

Hata hivyo, akizungumzia namna timu yake ilivyoanza vibaya kipindi cha kwanza, ikifungwa goli moja katika dakika ya 11, goli lililopachikwa na Callum Wilson, alisema kipindi chote cha kwanza kwake hakikuwa kizuri na kwamba walivyomaliza kipindi hicho wakiwa sare ya 1-1 alijiona kama kocha mwenye bahati zaidi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.

“Nadhani watu walioangalia mechi ya leo hawakuamini namna tulivyojiandaa vizuri wiki hii. Na katika kipindi cha pili mambo yalikuwa tofauti, ilikuwa haiwezekani kucheza vibaya zaidi ya ilivyokuwa kwenye kipindi cha kwanza. Timu ilifanya vizuri zaidi,” alisema.

Marcus Rashford (kushoto) akishangilia baada ya kufunga goli la ushindi dakika za nyongeza

Magoli ya Man United yalipachikwa na Anthony Martial katika dakika ya 35, huku Marcus Rashford akiwainua mashabiki wa timu hiyo katika dakika za nyongeza na kuifanya kubeba alama tatu muhimu.

Ushindi huo umeisogeza Man United katika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa Ligi, ikiwa na alama 20 sawa na Bournemouth iliyoko katika nafasi ya 6 ambayo imeizidi magoli ya kufunga.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 4, 2018
Serikali yatoa ufafanuzi wa taarifa ya balozi wa Umoja wa Ulaya ‘kufukuzwa’