Meneja wa Man Utd Jose Mourinho amewalaumu washambuliaji wake na kuwaita ‘Wazembe’ baada ya kushindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Anderlecht ya Ubelgiji katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali wa Europa League uliochezwa kwenye uwanja wa Constant Vendon Stock usiku wa kuamkia leo.

Man Utd walikuwa wanaongoza muda mrefu lakini wenyeji walisawazisha dakika ya 86 na kuufanya mchezo kumalizika kwa sare ya bao moja, hatua ambayo ilimkera Mourinho.

“Kama ningekuwa beki wa Man Utd ningekasirishwa sana na washambuliaji. Mabeki walifanya kazi kubwa lakini waliotakiwa kumaliza mchezo walishindwa.”

“Tatizo ni lile lile, tumecheza vizuri, tumetengeneza nafasi nyingi lakini tumeshindwa kufunga mabao,” alisema Mourinho.

“Katika kiingereza changu kibovu sijaona neno jingine la kuwaita washambuliaji wangu zaidi ya ‘Wazembe’. Wanapaswa kuongeza umakini zaidi.”

“Ukiangalia kiwango cha soka kilichoonyeshwa na wachezaji wawili ama watatu utaona haikuwa nzuri kabisa. Marcus Rashford, Jesse Lingard, Zlatan Ibrahimovic, Anthony Martial wote walikuwa sawa,” alimaliza Mreno huyo.

Henrikh Mkhitaryan aliifungia Man Utd dakika ya 36 ambapo Mashetani hao walipiga mashuti 16 langoni mwa wenyeji wao.

Man Utd wapo nyuma kimabao dhidi ya timu zote zilizo kwenye nne bora ya ligi kuu nchini England ambapo wamefunga mabao 46 huku timu za Chelsea, Tottenham, Liverpool, Manchester City na Arsenal wakifunga zaidi ya mabao 60.

Zlatan Ibrahimovic ndiye kinara wa timu hiyo baada ya kufunga mabao 28 huku wachezaji wawili tu Mkhitaryan na Juan Mata wakiwa wamefunga zaidi ya mabao 10.

Polisi Kenya watoa angalizo kwa wananchi, ni kufuatia taarifa za ujasusi
Azam FC Wabisha Hodi Tanga