Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, na bado yapo bandarini baada ya kushindwa kuyalipia kodi, yapigwe mnada na kwamba hajali vitisho vya mwanasiasa huyo kwani ameapa kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.

Mpango ametoa maamuzi hayo leo Jumatatu, Agosti 27, 2018 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alipofanya ziara ya kushtukiza na kukagua makontena hayo katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD).

Maamuzi hayo ya Dkt. Mpango yamekuja ikiwa ni siku mbili baada ya TRA kuyapiga mnada makontena 20 yaliyoingizwa nchini kwa jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  ambapo mkuu huyo jana alifanya ibada ya kumuomba Mungu yasipate wateja.

Makonda alishiriki ibada ya pili katika Kanisa la Anglikana, iliyoongozwa na Mchungaji Sabimbona Rushashi, mjini Ngara mkoani Kagera.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, akiwa wilayani Ngara kwenye msiba wa mama mkubwa wa mke wake, alisema sababu za kumfanya afanye ibada hiyo ni kuumizwa na kitendo hicho kilichofanywa na TRA wakati ikitambua makontena hayo si mali zake binafsi.

Alisema pia katika ibada hiyo, amewaombea walimu na wanafunzi wa mkoa huo na wananchi ambao wamejitolea kuchangia juhudi hizo za kujenga ofisi za walimu wasivunjike moyo.

“Amelaaniwa mtu yule atakayenunua furniture (samani) za walimu. Nimefanya ibada maalumu leo (jana) ya kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa sababu naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaofanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi,” alisema Makonda.

Juzi kontena moja la samani hizo lilikuwa  likiuzwa kwa Sh. milioni 60 wakati wateja waliofika kununua walifikia gharama ya Sh. milioni 30.

Kontena hizo ambazo zilipigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono Action Mart, zilikuwa na samani aina ya meza, viti na mbao za kufundishia wanafunzi.

Kontena hizo zinapigwa mnada kutokana na kushindwa kulipiwa kodi ya Sh. bilioni 1.2 zinazodaiwa na TRA baada ya kuwasili nchini.

 

NEC yawapiga msasa wasimamizi wa uchaguzi
Gattuso achukizwa na Bakayoko