Katika juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umasikini serikali imesema inaandaa mpango mkuu wa Taifa wa maendeleo ya sekta ya fedha utakaotumika kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, mitaji ya muda mrefu, kulinda watumiaji wa huduma za fedha na kuimarisha sekta hiyo.

Hayo yamebainishwa na Naibu waziri wa fedha na mipango Dkt. Ashatu Kijaji jijini Dodoma jana, wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau cha kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya mpango mkuu wa Taifa wa maendeleo ya sekta ya fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030.

Amesema serikali inaandaa mpango huo huku ikiendelea kutekeleza mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2016/17 unaoelekea kukamilika mwaka 2020/21 ambao ulikua na lengo la kujenga uchumi wa viwanda.

“Dhima kuu ya mpango huu ni uchumi wa viwanda utakaoenda bila kuwaacha nyuma watanzania na miongoni mwa vipaumbele ni kuondoa umasikini wa kipato kwa watu na uimara wa sekta ya fedha ambao ndio nyenzo muhimu ya uimara wa sekta ya viwanda,” amefafanua Dkt. Kijaji.

Kuhusu taasisi za huduma ndogo za kifedha zinavyowawezesha wanawake zipo 450 lakini ni asilimia 12 pekee ya kundi hilo ndiyo imefikiwa na taasisi hizo hivyo kikao kazi cha kujadili mpango mkuu wa Taifa wa maendeleo ya sekta ya fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030 utangalia njia muafaka ya kutatua tatizo hilo.

Aidha katika hatua nyingine Dkt. Kijaji amewataka watanzania ambao wamepata elimu ya bima kufungua kampuni za bima za ndani ili ziweze kuingia katika ushindani na kampuni za nje.

Amesema kampuni za bima zilizopo nchini ni 31 pekee na kati ya hizo za kitanzania hazizidi tatu na hivyo upo umuhimu wa jambo hilo ili wale waliopata elimu waweze kuanzisha ofisi za kitanzania ili kuwa na ushindani.

“Upo ulazima wa watanzania wenye elimu ya masuala ya bima kifungua kampuni za bima ili kuleta ushindani katika utoaji wa huduma za namna hiyo maana makampuni ya namna hii yapo 31 nchini lakini cha kushangaza za wazawa hazizidi tatu,” amebainisha Dkt. Ashatu.

Awali mchumi mkuu wa wizara ya fedha na mipango Dionesia Mjema alisema maagizo yote yaliyotolewa na Naibu waziri Dkt. Ashatu Kijaji yatafanyiwa kazi na makundi ya wadau wakiwemo wa benki, huduma za bima na kundi la sekta ndogo ya fedha.

Amebainisha kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wangalia namna ya kutatua changamoto za sekta ya fedha kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.

Mamilioni ya benki ya NJOCOBA yaanza kurejeshwa
LIVE: Rais Magufuli akifungua Mkutano wa Mawaziri Afrika na Nordic

Comments

comments