Serikali imewaondoa hofu watanzania kuwa nyama inayopatikana nchini ni bora na yenye usalama wa kutosha na kwamba kwa namna yoyote hawawezi kula vibudu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 30 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali8 la Mbunge wa Mbinga mjini Sixtus Mapunda aliyetaka kusikia kauli ya serikali kuhusiana na jaribio la kuuza vibudu katika machinjio ya Tegeta Jijini Dar es Salaam Mei 13, 2018.

Mpina amesema kuwa katika machinjio ya Tegeta walilikamata lori likiwa na Ng’ombe 54 kati ya hao 12 walikuwa ni mizoga ambapo mizoga hiyo minne ilikuwa imeshachunwa na miwili ilikuwa tayari imeshakatwa katwa vipande.

“Vyombo vyetu vya usimamizi, Mkurugenzi wa Mifugo, TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini) na Halmashauri tunao usimamizi madhubuti kwenye machinjio na mabucha yetu katika kuzingatia usalama wa walaji hivyo basi watanzania wote wasipewe mashaka wala hofu na mtu yoyote kwasababu nyama za Tanzania ni bora kwa namna yoyote hawawezi kula vibudu,”amesema Mpina

Aidha, Mpina amewashauri watanzania waendelee kula nyama za mifugo yao kwa kuwa vyombo vya dola vipo na vinawahakikishia usalama wa kutosha katika masuala hayo.

Hata hivyo, Mpina ameongeza kuwa mpaka sasa hivi serikali imewaondoa watumishi wote waliokuwa katika kizuizi cha Kibaha na kupeleka wengine baada ya tukio hilo.

Video: Makonda akutana na Wakandarasi jijini Dar
Serikali yachangia mamilioni kupunguza mimba za utotoni

Comments

comments