Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amepiga marufuku makongamano ya wafugaji yenye lengo la kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa uamuzi aliochukua wa kuwasaidia badala yake ametaka watumie kipindi hiki kifupi walichopewa kuainisha maeneo ambayo yamepoteza sifa za uhifadhi yaweze kuchukuliwa  kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi waishio Kando ya Hifadhi ya Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu mkoani Simiyu kwenye ziara ya Kamati ya mawaziri nane, ambapo Mpina amesema kuwa tangu mwaka 2000 tume zaidi ya 27 ziliundwa na Bunge na Serikali kushughulikia migogoro zaidi ya 1,095 lakini asilimia 99 ya mapendekezo ya tume hizo hayajatekelezwa mpaka sasa.

Amewataka wafugaji kote nchini kujipanga na kupendekeza maeneo yaliyopoteza sifa za uhifadhi, mashamba yasiyoendelezwa ili wafugaji waweze kupatiwa kwa ajili ya malisho ya mifugo yao kama sehemu ya kuunga mkono uamuzi uliotolewa wa kusaidia sekta hiyo.

Amesema kuwa tume nyingi zilizoundwa miaka ya nyuma kushughulikia migogoro hiyo zilichakachuliwa hata kabla ya kukabidhi matokeo ya mambo waliyobaini kwa kuwa kwenye migogoro hiyo wako baadhi ya viongozi wa Serikali.

Aidha, amesema kuwa baadhi ya watendaji wa Serikali walilazimika hata kutoa rushwa ili kubadilisha maamuzi ya tume zilizokuwa zinaundwa kushughulikia migogoro hiyo kwa sababu wananufaika na migogoro hiyo.

“Rais Magufuli aliamua kuunda tume ambayo haitapokea rushwa,ambayo ni timu ya Lukuvi mnaiona ina sura ya kupokea rushwa, hapa hakuna mtu anayefanana na kupokea rushwa, tupo kwaajili ya kutatua migogoro hii,”amesema Mpina

 

Hata hivyo, Mpina amewahakikishia kuwa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi yatafika kwa Rais tofauti na tume zingine zilizotangulia zilikuwa hazina uwazi wa namna ya kuchukua maoni na namna ya kufikisha mapendekezo serikalini.

 

Mawaziri wanaounda timu hiyo mbali na Mpina na Lukuvi ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suleiman Jafo, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mussa Sima.

Baada ya kushushiwa kipigo kutoka kwa Simba, Yanga na Azam FC kushuka dimbani tena
Majaliwa azitaka benki kupunguza riba za mikopo