Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina, leo ametembelea katika Maeneo ya Keko Magurumbasi na kujionea namna ambavyo wamiliki wa viwanda wanavyotiririsha maji katika mfereji wa mseleleko uliopo maeneo hayo.

Aidha, Mpina amewataka wawekezaji wenye viwanda nchini waliojenga juu ya miundombinu ya majitaka kubuni njia nyingine ya ujenzi sahihi wa miundombinu ya majitaka kutoka viwandani mwao kwenda kwenye mfumo wa mamlaka za maji ili kuepusha uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo, Mpina amesema kuwa, wamiliki wa viwanda watakaoendelea kuchafua mazingira watachukuliwa hatua kali huku oparesheni kubwa ikifanyika nchini nzima ya ukaguzi wa mazingira itakayohusisha halmashauri za miji, mamlaka za maji, wamiliki wa mabomba ya maji taka na wananchi ili kuwajibika kwa pamoja katika kunusuru uharibifu wa mazingira.

Vilevile, Mpina ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kuiandikia hati ya zuwio TANROADS ya mwezi mmoja inayowataka wafumue karavati lao linalopita chini ya barabara katika eneo la kurasini BP darajani na kuliongeza ukubwa ili majitaka yaweze kupita kwa nafasi.

Kwa upande wake mratibu wa Mazingira wa kanda ya mashariki kutoka NEMC,  Jaffari Chimgege amesema wao kama Baraza watakaa kwa Pamoja na wawekezaji, wenye makaravati madogo yanazoshindwa kupitisha majitaka vizuri jijini DSM na kutafuta suluhisho la kudumu kwani hali hiyo ni hatari hasa katika kipindi cha mvua, inaweza kusababisha magojwa ya milipuko kama vile kipindupindu.

Video: Umasikini kwa wasanii Bhaasi..! Rais TCDB ataja mipango mikubwa
Mahakama yawafutia kesi viongozi wa Chadema