Mgombea wa Upinzani, Martin Fayulu amedai kuwa anaamini ameshinda uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kwamba hatakubali majadiliano ya matokeo halisi.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Congo (Ceni) ni lazima itangaze matokeo ya uchaguzi wa urais mapema iwezekanavyo. Matokeo haya ya uchaguzi sio ya majadiliano,” BBC imemkariri Fayulu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Corneille Nangaa ameeleza kuwa kutotangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo Jumapili kama ilivyokuwa imeahidiwa kunatokana na kutokamilika kwa zoezi la kuhesabu na kujumlisha kura kwenye vituo kadhaa.

Hivi karibuni, Kanisa Katoliki ambalo lilisambaza waangalizi 40,000 katika vituo vya kupigia kura lilieleza kuwa tayari linamfahamu mshindi wa uchaguzi huo. Kauli hiyo ililaaniwa vikali na Serikali inayoongozwa na Rais Joseph Kabila ikieleza kuwa hilo sio jukumu la Kanisa.

Mgombea wa chama tawala anayeungwa mkono na Rais Kabila, Emmanuel Shadary ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Fayulu ambaye alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa mafuta pamoja na Felix Tshisekedi ambaye ni mtoto wa kiongozi wa zamani wa upinzani.

Wiki iliyopita, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa vikosi 80 vya jeshi vimetumwa karibu na Gabon kama sehemu ya maandalizi endapo kutatokea vurugu za uchaguzi DRC.

Alieleza kuwa vikosi hivyo vitaingia DRC itakapobidi kwa lengo la kuwalinda raia wa Marekani pamoja mali zilizopo kwenye ofisi za kidiplomasia katika Mji Mkuu wa Kinshasa.

Kwa mujibu wa Military Times, Ikulu ya Marekani imepanga kutuma vikosi zaidi kutokana na hali itakavyoendelea kuonekana kutokana na taharuki iliyozuka kufuatia uchaguzi huo.

Uchaguzi huu utafanikisha kumpata mrithi wa Rais Kabila ambaye ameongoza kwa miaka 18. Utakuwa uchaguzi wa kidemokrasia wa kumpata kiongozi mpya tangu nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1960 kutoka kwa Ubelgiji.

Cheka afunguka uchawi kwenye ndondi
CAG mstaafu ajibu kitendawili cha Spika kumuita CAG kwa hiari, kwa pingu