Kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Martin Fayulu ameandika barua kwa Umoja wa Afrika akitaka uchaguzi wa Desemba 2018 urudiwe ndani ya miezi sita.

Fayulu amekuwa akisisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi huo yalipikwa na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mshindi na sio Rais Filex Tshisekedi.

Barua hiyo ya Fayulu aliielekeza katika Mkutano wa 32 wa Wakuu wa nchi za Afrika, uliofanyika wikendi iliyopita jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mfanyabiashara mkubwa wa mafuta, aliiweka barua hiyo iliyoandikwa Februari 8 kwenye akaunti yake ya Twitter. Barua hiyo yenye ujumbe mzito kwa wakuu wa nchi, imejaa baadhi ya mambo ambayo amekuwa akiyalalamikia. Fayulu anadai kuwa uchakachuaji wa kura za Urais unampa wakati mgumu Rais Tshisekedi kumpata Waziri Mkuu kwani viti vya ubunge alivyonavyo havitoshelezi.

Rais Tshisekedi alihudhuria kikao hicho cha wakuu wa nchi, kikiwa kikao chake cha kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais wa DRC.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI), Tshisekedi alipata asilimia 38 ya kura zote, akifuatiwa na Fayulu aliyepata asilimia 34.

Fayulu amekuwa akieleza kuwa alishinda kwa kishindo uchaguzi huo, akiwa na asilimia 60. Mahakama ya Kikatiba nchini humo ilitupilia mbali ombi lake la kutaka matokeo hayo ya uchaguzi yabatilishwe na kuitisha uchaguzi mpya.

Serikali yabaini pipi, vidonge vyenye dawa mpya za kulevya
Video: Vigogo CCM wamtega Magufuli, Mmiliki mwendokasi kortini tuhuma nzito