Mpinzani mkuu wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Dk. Kizza Besigye ambaye amekuwa akipinga ushindi wa Rais huyo, amedaiwa kujiapisha kuwa Rais.

Taarifa zinaeleza kuwa Besigye amejiapisha jana ikiwa ni siku moja tu kabla Rais Museveni hajaapishwa rasmi (leo) katika sherehe ambayo itahudhuriwa na marais wan chi 14 za Afrika ikiwa ni pamoja na Rais John Pombe Magufuli.

Wafuasi wa Besigye walikutana kwa wingi jijini Kampala Uganda mapema asubuhi kwa ajili ya kushuhudia tukio la kuapishwa kwa mwanasiasa huyo, kiapo ambacho hakitambuliki kisheria.

Hata hivyo, Polisi nchini humo wamemshikilia Besigye kwa mahojiano kutokana na tukio hilo. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Yoweri Museveni kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliopita akiwaacha kwa mbali wapinzani wake wakuu, Kizza Besigye na Amama Mbabazi.

Kadhalika, Mahakama Kuu nchini humo ilihalalisha ushindi wa Museveni baada ya kutupilia mbali shauri la pingamizi la ushindi huo lililowasilishwa na Amama Mbabazi.

Ndanda FC: Young Africans Hawajatupa Pesa Yoyote
Chadema wabeza utumbuaji majipu wa Magufuli, wadai bora Kikwete

Comments

comments