Hatimaye timu ya washiriki wa mashindano ya Kili Challenge yaliyoandaliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushrikiana na TACAIDS na mashirika mengine, wamefanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro.

Timu hiyo ya wapanda mlima walioshiriki mashindano hayo yaliyolenga katika kuhamasisha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi ikiwa na watu 57 kutoka mataifa mbalimbali duniani imekamilisha ndoto yake leo. Hata hivyo, mshiriki mmoja alishindwa kufika katika kilele cha Uhuru kutokana na kuzidiwa na baridi.

Timu hiyo imekamilisha jumla ya mwendo wa Kilometa 460 ambazo ni umbali unaokaribia safari ya kutoka Moshi hadi jijini Dar es Salaam, ndani ya siku 7.

Kili Challenge

“Tunawapongeza wote waliopanda mlima pamoja na waendesha baiskeli kwa moyo wao wa kujitoa kwa ajili ya jambo lenye tija. Ushiriki wao katika shindano hili la mwaka huu lina maana kuwa walitakiwa kuziacha familia zao, wenza wao, kazi na kila kitu na kuweka muda wao na nguvu zao kwa ajili ya tukio hili,” imeeleza taarifa ya GGM.

Naye Mrisho Mpoto ametumia uzoefu alioupata katika safari hiyo kuwatia moyo wote wenye malengo mbalimbali kutokata tamaa kwani wanaweza kufanikisha endapo watajituma na kuweka nia.

“Ukiona rafiki anakwambia vitu vya kukukatisha tamaa usiende mbele, mbadilishe haraka sana hafai kabisa!! #Mpotokileleni,” Mpoto ameandika kwenye akaunti yake ya Instagram.

“Kwenye maisha endelea kujaribu kila kunapokucha ipo siku tu.#Mpotokileleni,” aliongeza kwenye picha nyingine.

Video: Cassim Mganga akitumbuiza katika Tamasha la ZIFF Zanzibar
Madee awataka BASATA kuwa wabunifu zaidi, “adhabu zao haziathiri wasanii”