Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) imetangaza nafasi za kazi 10,000 kwa wananchi wote waliopo nchini kwenye mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutokea Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga utakao igharimu Serikali Dola za kimarekani Bilioni 3.5 sawa na Shilingi Trilioni 8 za Kitanzania.

Taarifa hiyo imeelezwa na  Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaESA, Boniface Chandaruba akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kuwataka watanzania kujitokeza kujisajili na ajira hizo.

Amesema kuwa zoezi la usajili wa ajira  tayari limekwishaanza na litasitishwa rasmi Machi 30, 2018, na kusema kwamba usajili wa nafasi hizo za kazi hauna gharama yeyote lengo likiwa ni kuwatambua rasmi waajiriwa hao.

”Tanzania inayo fursa kubwa ya ajira katika mradi huu wa ujenzi wa bomba la mafuta hivyo sisi kama TaESA tumepewa jukumu la kuwahamasisha watanzania waweze kujitokeza na kujisajili TaESA ili serikali iweze kubaini wananchi wenye ujuzi na sifa za kuweza kufanya kazi kwenye mradi huu wa bomba la mafuta na gesi”, amesema Chandaruba.

Aidha, Mradi huo unatarajiwa kuchukua kati ya miezi 24 hadi 36 na unategemewa kuzalisha fursa za ajira takribani 10,000 wakati wa ujenzi na ajira zaidi ya 1,000 wakati wa uendeshaji wake.

Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi  “East Africa Crude Oil Pipeline (EACOP)”  kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania unategemewa kuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo ujenzi wa kilometa 1,115 za bomba hilo utafanyika nchini Tanzania. Jumla ya wilaya 24 na vijiji 184 hapa nchini vinategemewa kupitiwa na bomba hilo katika mikoa 8 ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Abdul Nondo awachanganya Polisi
Uchaguzi wa rais kurudiwa Siera Leone