Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA, kupitia idara ya Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa Gombe, imekabidhi vifaa kwa ajili ya mradi wa ufugaji nyuki vyenye thamani ya shilingi 31 milioni kwa vikundi vitatu vyenye jumla ya wanachama 73.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Gombe,
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Yustin  Njamasi amesema mpango huo ulioibuliwa ukilenga utunzaji wa minimum ya Hifadhi na Mazingira, utahusisha vikundi viwili kwa Kijiji cha Mwamgongo na kikundi kimoja katika Kijiji cha Kiziba Mkoani Kigoma.

Amesema  “mradi huu ulihusisha utoaji wa semina ya ufugaji nyuki kisasa,vifaa vya ufugaji na kununua mizinga (160), mashine(4) za kukamulia asali, malazi (16) ya ufugaji nyuki, pamoja na viti a moshi (4) kwa wanavikundi hao.”

Aidha, Kamishna Njamasi, alibainisha kuwa shughuli za ujirani mwema zimekuwa zikifanyika kwa miaka mingi tangu miaka ya tisini kwa ushirikiano mkubwa kati ya Hifadhi ya Taifa ya Gombe na vijiji jirani vinavyopakana moja kwa moja na Hifadhi pamoja na vile vinavyo changia Mfumo wa ikolojia moja na Hifadhi ya Taifa ya Gombe.

Akikabidhi mradi huo kwa wanakikundi hao, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Salum Abdallah Kalli, aliwaasa wananchi kushirikiana na Hifadhi katika kutunza rasilimali hizi kwa faida ya sasa na ya baadae

“Niwatake wananchi wote kushirikiana na Hifadhi katika maswala mazima ya ulinzi wa misitu na Wanyamapori hususani Sokwemtu pamoja na vyanzo vya  maji pia mtunze mradi huu ili kuweza kuwapatia faida za kiuchumi na kimazingira”. alisema Kalli.

Aidha  Kalli pia alitoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kuzitembelea Hifadhi hususani Hifadhi ya Taifa Gombe ili kuweza kujionea vivutio lukuki vilivyomo katika hifadhi hizo pamoja na kuchangia pato la Taifa.

TANAPA kupitia idara ya Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Gombe imetekeleza miradi mbalimbali iliyoibuliwa na wananchi ambayo imelenga katika utunzaji wa Mazingira kama Ufugaji nyuki, mfumo wa umeme jua kwa vikundi vya uvuvi kwa lengo la utunzaji wa fukwe na mazalia ya samaki kuzunguka fukwe za ziwa Tanganyika kuepusha matumizi ya mafuta ya taa ambayo husababisha uchafuzi wa ziwa.

Katika hatua nyingine, TANAPA pia imetekeleza miradi ya kimaendeleo kama Ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Bugamba, Ujenzi wa Madarasa matatu katika Shule ya Sekondari Bugamba, Ujenzi wa Madarasa mawili katika shule ya Msingi Mwamgongo, pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu (Two in One)-katika Kijiji cha Mwamgongo, Miradi ambayo  imegharimu zaidi ya shilingi 230 milioni.

Odinga azionya nchi za Magharibi kuingilia mambo ya Kenya
Makamu wa Rais Marekani awasili nchini