Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba ambaye jana ameanza kufanya usafi katika hospitali ya Sinza Palestina jijini Dar es Salaam kama sehemu ya adhabu yake ya kifungo cha nje, ameishauri serikali kuwatumia wafungwa katika kazi za jamii badala ya kuwaweka jela.

Akiongea na waandishi wa habari katika eneo lake la kufanyia usafi, Mramba ameeleza kuwa magereza sio sehemu salama na wala sio sehemu ya kumrekebisha mhalifu. Hivyo, aliishauri serikali kuanza kutumia sheria namba 6 ya huduma kwa jamii kuwatumia wafungwa wenye taaluma na fani mbalimbali kuihudumia jamii.

Waziri huyo aliyetoka jela na kuanza kutumikia kifungo cha nje, alitahadharisha kuwa jela sio sehemu sahihi zaidi ya kurekebisha tabia za watu bali inaweza kuwa sehemu hatari ya kuwafunza mbinu wahalifu wengine.

“Unakuta mtu amefanya uhalifu kwa kuiba kitu fulani, anafungwa na kupelekwa gerezani, anakutana na majambazi sugu wanaompa mbinu zaidi, sasa akitoka jela anakuja akiwa ameiva. Anarudi kwenye matukio akiwa ameiva zaidi,” Mramba alieleza.

Maoni ya Mramba yaliungwa mkono na Afisa Huduma za Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Deogratius Shirima ambaye alitoa wito kwa vyombo husika kuanza kutumia sheria ya huduma za jamii, namba 6 ya mwaka 2002 inayoruhusu kutumikia kifungo cha nje.

“Sheria hii ni vyema ikatumika kwa wale inaowagusa kwa sababu itasaidia kupunguza gharama za kuwahudumia kuanzia chakula, malazi na hata afya zao,” alisema Shirima.

Mramba na Daniel Yona (Waziri wa zamani wa Nishati na Madini) walihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya kutumia vibaya madaraka.

Hata hivyo, Februari 6 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilieleza kuwa ilipokea barua ya Magereza inayopendekeza wawili hao kutumikia kifungo cha nje kwa mujibu wa Sheria ya huduma kwa jamii. Mahakama iliridhia mapendekezo hayo na kuwataka wafanye usafi kwa saa nne kila siku katika maeneo ya hospitali ya Sinza Palestina kama sehemu ya adhabu hiyo.

 

Serikali: Hatukuihonga mahakama
Unataka kumjua mchawi wako kazini? Soma hapa