Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba ambao wanatumikia kifungo cha nje pamoja na kufanya usafi katika hospitali ya Sinza Palestina jijini Dar es Salaam, wamepewa kazi nyingine ya kusaidia kuongeza ufanisi ofisini.

Mawaziri hao wa zamani sasa wamepangiwa kazi ya kutoa ushauri elekezi wa kitaalam katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na masuala ya bajeti.

Afisa Mazingira wa Hospitali hiyo, Miriam Mongi, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Yona na Mramba ambao ni wataalam wa masuala ya uchumi na wazoefu, watakuwa wanapangiwa kufanya kazi nyingine za kitaalam katika idara za hospitali hiyo, ingawa kazi iliyopewa kipaumbele ni usafi wa mazingira.

Hivi karibuni, Yona na Mramba waliishauri Serikali kuwatumia wafungwa wenye utaalam kutumikia jamii na kushiriki katika kazi za maendeleo badala ya kuwafungia jela pekee na kuwahudumia kwa kiasi kikubwa cha fedha.

Katika hatua nyingine, Mongi alieleza kuridhishwa na namna ambavyo Mramba na Yona wanafanya kazi ya usafi wa mazingira katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuwahi katika eneo la kazi na kuitekeleza kwa kiwango kinachoridhisha.

Alisema kuwa ujio wa wawili hao katika hospitali hiyo, umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa wafanya usafi na kwamba mawaziri hao wamekuwa wakifanya kazi kwa moyo na wanaonekana wameikubali kazi yao.

“Hata ukizungumza nao na wanavyofanya kazi zao wanaonekana wamekubali majukumu yao na wameshazoea,” alisema Mongi.

Alibainisha kuwa mwendesha mashtaka huwatembelea na kuona namna ambavyo wanatekeleza adhabu yao ya kifungo cha nje na kufanya kazi za jamii, na ameonekana kuridhishwa na jinsi wanavyotekeleza majukumu yao.

Wenger Kumvisha Kitambaa Petr Cech
Matokeo ya kidato cha nne 2015 yatoka, yako hapa