Mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema ameweka wazi jinsi timu yake ilivyowahi kufoji sakata la ufisadi dhidi ya Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Mheshimiwa Benjamin Mkapa, kwa lengo la kujipatia umaarufu.

Akizungumza leo kwenye mahojiano na kipindi cha Maisha Mseto cha Times FM, Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, amesema kuwa kuna wakati vyama vya upinzani kwa lengo la kujipatia umaarufu, hutunga kashfa dhidi ya Serikali na viongozi wake kama yeye na timu yake walivyowahi kufanya miaka ya 1990.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa anakumbuka mwaka mmoja baada ya kutoka kwenye uchaguzi, walifoji barua na kutunga dhidi ya Serikali kuwa viongozi wa juu na hadi kumtaja Mheshimiwa Mkapa kuwa  alifanya ufisadi wa sh.900 milioni.

“Lile tukio la Mh. Mkapa kwamba amekula Milioni 900, tulitengeneza sisi ili kumnyima sifa Mheshimiwa Mkapa na wananchi watuamini sisi watupe nafasi,” alisema.

Alifafanua kuwa timu yake kwa pamoja walikubaliana kuwa kwakuwa yeye ndiye aliyekuwa na ushawishi zaidi kwa wananchi alibebe sakata hilo ‘feki’ na alifanya hivyo; alisema “tulipanda kwenye majukwaa na barua ile ya kufoji na tukawa tunahoji kuhusu fedha zile.”

Mwanasiasa huyo ambaye miaka ya 1990 alikuwa kiongozi wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa zaidi akigombea urais tangu mwaka 1995, alisema kuwa hadi sasa baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikitunga matukio ya kuichafua Serikali na hata Rais kwa lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Wakati huo, Mrema alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, chama ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani.

Katika hatua nyingine, Mrema alisifu kazi inayofanywa na Rais John Magufuli na kueleza kuwa ndani ya muda mfupi Serikali yake imefanikiwa kupambana na ufisadi kwa kiasi kikubwa.

Alisema alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alijaribu kupambana na ufisadi, hali iliyosababisha achukiwe na wengi, lakini hakufanikiwa kama alivyofanikiwa Rais Magufuli.

“Unajua ili ufanikiwe kwa baadhi ya mambo ya nchi ni lazima uwe Rais kwakuwa unakuwa wewe ndiye muamuzi wa mwisho. Mimi nilishindwa kwa sababu wakati mwingine unakuwa unafanya jambo lakini lisipoungwa mkono na walio juu yako huwezi kufanikiwa,” alisema.

“Sasa hivi mwenye nchi ndiye anayepambana na ufisadi. Atafanikiwa kwa sababu yeye ndiye anayesimamia kuliko wakati wangu mimi sikuwa na Serikali,”  Mrema aliongeza na kutoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu na kumsikiliza Rais John Magufuli.

Akizungumzia mpango wa kugombea ubunge katika jimbo la Vunjo kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, Mrema alisema atawasikiliza wananchi wa jimbo hilo ambao amedai wanalalamika kwa kukosa maendeleo baada ya kutomchagua.

Mrema alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 alipokuwa akitetea kiti chake cha ubunge wa Vunjo na nafasi yake ikachukuliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kupitia Ukawa.

Samia Suluhu aipongeza CCBRT kwa kurudisha heshima ya mwanamke
Urusi yadokeza itakachofanya kuhusu mkutano wa Trump na Kim