Mwenyekiti wa Parole, Augustino Mrema amemshukia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kuwa anafanya makosa makubwa kutetea watuhumiwa wa dawa za kulevya.

Mrema amesema anamshangaa Lissu kuwatetea watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na kumshauri atumie elimu yake ya sheria kuwatetea waathirika na wanaotaja wahusika wa dawa za kulevya akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Mbali na Lissu, Mrema ameigeukia  mahakama na kusema kuwa itambue kuwa pamoja na kutafsiri sheria, jukumu la kuzuia dawa za kulevya lipo mikononi mwao.

“Nashangazwa na hawa wanaotuhumiwa kukataa kwenda kupimwa na kuonyesha juhudi za kuzuia zoezi hilo, wakubali kwenda kupimwa kwani ndio itakuwa kusafishwa kwao kama majibu yatatoka kuwa hawatumii,” amesema Mrema.

Kwa upande wake, Lissu amesema Mrema anapaswa kujiuzulu cheo alichopewa cha Mwenyekiti wa Parole kwa sababu alipewa kinyume cha sheria.

Amesema sheria ipo wazi kwamba Mwenyekiti wa Parole awe jaji au alishawahi kuwa jaji na si mwanasiasa kama Mrema.

“Ninapoona Mrema anapiga kelele, anatetea chakula chake na si vinginevyo, kisheria Mwenyekiti wa Palore anapaswa kuwa jaji au alishawahi kuwa jaji,”amesema Lissu.

Hata hivyo, kuhusu kuwatetea watuhumiwa, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, amesema sheria ipo wazi kwamba wanachofanya mawakili kwa sasa ni kuwatetea watuhumiwa wote hata wanaotuhumiwa na dawa za kulevya, kwani sheria inamtaka wakili kutetea yeyote bila ubaguzi.

Jeshi nchini Guatemala kupiga marufuku utoaji mimba
Samia suluhu asisitiza ushirikiano bonde la mto Nile