Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labor Party (TLP), Augustine Mrema ameunyooshea kidole mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kufanya maandamano nchi nzima Septemba 1, kupitia Operesheni waliyoipa jina la UKUTA.

Akizungumza muda mfupi baada ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutangaza kuvialika vyama vya siasa kwenye Baraza la Vyama vya Siasa kwa lengo la kufanya mazungumzo kuhusu hali ya kisiasa nchini, Mrema amekosoa mpango huo akidai umelenga kuwabembeleza Chadema.

Mrema alionesha kukubali kwa shingo upande kushiriki mazungumzo hayo akidai kuwa amefanya hivyo kwa kumheshimu Msajili huyo na sio vinginevyo.

“Mazungumzo ya Chadema hayana tija kwa sababu lengo lao sio zuri. Huu mkutani ni wa kuwabembeleza tu Chadema. Sisi (TLP) tutaenda tu kwa heshima ya Msajili,” Mrema anakaririwa.

Tofauti na mtazamo wa Mrema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia yeye alikosoa uamuzi wa wa Msajili kuitisha mkutano na Baraza la vyama vya siasa akidai kuwa alipaswa kuhimiza vyama na watawala kuheshimu Katiba ya nchi.

Alidai kuwa Chadema wanachokifanya ni halali kikatiba  na kwamba Msajili anajua hilo, “Msajili ajitokeze atangaze kuwa Katiba iheshimiwe tutamuelewa.”

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji ameeleza kuwa chama chake hakioni umuhimu wa kukaa kwenye mazungumzo kwa sasa kwa sababu Septemba 1 sio siku ya vurugu kama ilivyoelezwa na watu wengine.

“Anataka meza ya mazungumzo kwa ajili gani? Je, ni ya upatanisho wa lipi? Hapa msajili nadhani angefunguka zaidi ili tumuelewe,” alisema Dk. Mashinji.

Video: Wapenzi wa jinsia moja 'wazaa' mapacha watatu
Lowassa awatuliza wafuasi wa Chadema