Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema ameainisha tofauti  za kiutendaji kati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Wilbroad Slaa na Katibu Mkuu wa sasa Dk. Vincent Mashinji.

Dk. Vicent Mashinji

Dk. Vicent Mashinji

Dk. Mashinji alishika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini miezi michache baada ya Dkt. Slaa aliyekuwa na ushawishi mkubwa kung’atuka akipinga kitendo cha chama hicho kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kuwa mgombea urais akiungwa mkono na vyama vilivyounda Ukawa.

Akibainisha tofauti hizo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mrema alieleza kuwa mtindo wa uongozi wa Dk. Mashinji ni bora zaidi ya ule wa Dk. Slaa kwani Katibu Mkuu huyo kwanza huhangaika kushughulikia chanzo cha tatizo wakati anapambana na tatizo, wakati Dkt. Slaa alikuwa anaenda moja kwa moja kulitibu tatizo kabla ya kushughulikia chanzo.

Kadhalika, Mrema alieleza kuwa wakati Dkt. Slaa alikuwa anapenda kuongea na waandishi wa habari kwa niaba ya chama mara nyingi, Dk. Mashinji amekuwa akitoa nafasi zaidi kwa wasaidizi wake kufanya hivyo.

“Kazi ya Katibu Mkuu wa chama ni kukipanga chama na ndicho anachokifanya Dk. Mashinji. Halafu kitu kingine Dk. Mashinji anatengeneza vipaji na timu ya watu watakaoisaidia Chadema baadae,” Mrema anakaririwa na gazeti la Mwananchi.

Mrema ambaye katika uchaguzi wa mwaka jana alikuwa Meneja kampeni wa Mgombea wa Chadema na Ukawa kwa ujumla, Edward Lowassa, ametajwa pia kuwa ni mmoja kati ya wachora ramani wa oparesheni za Chadema ikiwa ni pamoja na oparesheni UKUTA iliyopangwa kufanyika Septemba 1 mwaka huu.

Hata hivyo, Rais John Magufuli amepiga marufuku kufanyika kwa maandamano na mikutano akiwataka wasimjaribu.

Wimbo Mpya: Young Killer - Mtafutaji
Nay wa Mitego kafunguliwa, 'Pale Kati' bado kifungoni