Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Tanzania, Augustine Mrema amesema kuwa  uhalifu unaoendelea kujitokeza hapa nchini unafanywa kwa makusudi na watu wenye nia mbaya na Serikali ya awamu ya Tano.

Amesema kuwa uhalifu kama huo haukubaliki hivyo unatakiwa kupigwa vita na kila mtu mwenye mapenzi mema na nchi kwani haijawahi kutokea mauaji ya askari Polisi kama yaliyotokea hivi karibuni.

Ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo kimoja cha redio Jijini Dar es salaam kuhusu hali ya nchi ilivyo kwa sasa, amesema kuwa kwa sasa ana mpango wa kuonana na Rais Dkt. Magufuli ili aweze kumuomba amruhusu kutoa wafungwa wenye sifa ya kupata msamaha ili waweze kusaidia kutoa taarifa za watu wanaofanya uhalifu huo.

“Kuwatoa wafungwa wenye sifa ya kupata msamaha itakua ni moja ya mkakati ambao utawezesha kukamatwa kwa wahalifu wanaondelea kufanya mauaji nchini, hawa wafungwa lazima watakuwa wanajua walipo wahalifu,” amesema Mrema.

Aidha, Mrema ameongeza kuwa atatumia mbinu zote na uzoefu alionao ili kuweza kupambana na uhalifu huo, kwani kulingana na uzoefu wake amegundua kuna kampeni za makusudi zinazofanywa kwa ajili ya kumchafua Rais Dkt. Magufuli.

Hata hivyo, katika hatua nyingine amemtaka Rais Dkt. Magufuli kuwashughulikia wale wote wanaoleta viashiria vya uvunjifu wa Amani hapa nchini.

 

Magazeti ya Tanzania leo April 25, 2017
Video: Mapambano Dawa za Kulevya, viongozi wa dini waombwa kuunga mkono