Msanii wa muziki wa asili nchi, Mrisho Mpoto ambaye pia ni mmoja kati ya wasanii ambao wanatoa elimu kwa jamii juu ya kukomesha suala la mauwaji ya tembo nchini, ameipokea kwa furaha hatua ya nchi ya China kutaka kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo nchini humo.

Katika matembezi ya amani ya kupinga ujangili hapa nchini yaliyofanyika leo Januari 14, 2016, Balozi wa China, Lu Youqing amesema nchi ya China ipo kwenye mkakati wa kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo na wanatarajia mwishoni mwa mwaka huu biashara hiyo kufa kabisa.

Akiongea na waandishi wa habari kuhusu kauli hiyo, Mrisho Mpoto amesema hatua hiyo ni nzuri na itasaidia nchi mbalimbali duniani kuiga nyayo zao.

“Mimi ni mmoja kati ya wasanii ambao tumekuwa tukihusika sana katika hizi harakati hasa hasa kimataifa zaidi, nimeshasafiri nchi mbalimbali kama mtanzania kupinga mauwaji ya tembo au ujangili ndio maana hata leo nipo kwa baada ya kualikwa na ubalozi wa China kwamba wameona jitihada zangu,” amesema Mpoto.

Mrisho amesema kuwa hatua ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo ni kitu kizuri sana kwa sababu huu ni mwanzo kwa China ambao zimekuwa zikisema China ndo vinara wa biashara hiyo kuwa na mtazamo mwingine, lakini pia kupitia maamuzi haya naona sasa biashara hii inaenda ukingoni kama nchi zingine za Ulaya ambazo zimekuwa zikitajwa kufuata msimamo wa China,”

Amesema suala la kupinga ujangili nchini sio suala la mtu mmoja, kila mtanzania ana haki ya kulinda maliasili za nchi kwajili ya kizazi kijacho.

Pia muimbaji huyo ambaye bado anafanya vizuri na wimbo Sizonje, amesema yeye bado ataendeleza mapambano kwa kuanzisha kampeni mbalimbali ambazo zitawafanya watanzania kufichua majangili kwa kuwa ni watu ambao wanatoka katika jamii zetu.

Chadema wajipanga kumtoa Lema,waandaa mawakili 18
Mashindano ya vikundi vya mazoezi kuanza jijini Dar es salaam