Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Shadrack Kapanga (34) kwa tuhuma za mauaji ya mama na watoto wake wawili eneo la Masaki mtaa wa Maryknol.

Kapanga ambaye ni msaidizi wa kazi za ndani alikamatwa jana Ijumaa Juni 11, 2021 eneo la Magomeni akiwa kwenye harakati za kutoroka baada ya kuwaua Emilly Mutaboyerwa ambaye ni mama na Damita (13) na Daniela Mutaboyerwa (15).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Juni 12, 2021 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na baadhi ya vitu alivyoviiba baada ya kufanya tukio hilo.

“Vitu alivyokutwa navyo wakati akitoroka ni simu za marehemu, televisheni, king’amuzi cha DSTV na rimoti,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Muliro ameeleza kuwa upelelezi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo la mauaji Juni 9, 2021 baada ya kuwapiga kila mmoja kwa wakati tofauti kwa kitu kizito na kuwasababishia kuvuja damu nyingi na kupoteza maisha.

“ Baada ya kuwaua aliwafungia ndani na kutoroka. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili kujua sababu za msingi za mauaji hayo na mara utakapokamilika mhusika/wahusika watafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo,” inaeleza taarifa hiyo.

Ajira kwa watoto yapindukia
Serikali yapiga 'stop' vivuko viwili kufanya safari