Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa nchini imesema kuwa itaendelea kukichukulia hatua za kisheria Chama Cha ACT-Wazalendo endapo hakitajibu barua yake ndani ya siku 14, kuanzia Machi 15, 2019.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amekanusha taarifa zilizokuwa zikidai kuwa hatua za ofisi hiyo dhidi ya chama hicho zinatokana na Maalim Seif Sharif kujiunga na chama hicho.

Amesema kuwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya chama hicho ni za kisheria kwakuwa kuna uvunjifu wa kifungu cha 5 na 6 cha Sheria ya Vyama Vya Siasa na sio vinginevyo.

Alieleza kuwa hatua hiyo sio ya kwanza kuchukuliwa nchini dhidi ya vyama vya siasa, kwani mwaka 2016 vyama vingi viliandikiwa barua ya kujieleza kwanini visifutwe kwa kushindwa kuwasilisha taarifa za matumizi ya fedha, na kuna baadhi ya vyama vilivyoshindwa kufanya hivyo vilifutiwa usajili.

“Katika kipindi hicho, Chausta, APPT-Maendeleo na Jahazi Asilia vilifutwa. Lakini hakuna chama chochote cha siasa ambacho kilijitokeza kujibu barua zetu kwenye vyombo vya habari. Wote walijibu kwa maandishi, hali ambayo tulitarajia ACT wafanye hivyo pia,”  Nyahoza aliiambia The Citizen.

Aliongeza kuwa hata mwaka jana, ACT walipewa barua kama hiyo lakini ilihitaji maelezo kuhusu taarifa za matumizi ya fedha kwa Mwaka 2013/14.

Akizungumzia kuhusu kujibu barua ya Msajili, kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuwa jana chama hicho kiliwasilisha majibu yake kwa Msajili kujibu hoja zote zilizotakiwa.

ACT-Wazalendo ina mbunge mmoja na inaongoza Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa na madiwani 19 kati ya 26.

Video: Zitto Kabwe apagawa, JPM aishukia TRA
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Aprili 2, 2019