Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru amesema kuwa uamuzi wa baadhi ya taasisi za umma kuweka fedha kwenye akaunti maalum (fixed deposit account) kwa lengo la kuzizalisha sio ‘dhambi’.

Mafuru ameyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli kuivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuridhia Mamlaka hiyo kuweka kiasi cha shilingi bilioni 28 kwenye fixed ‘deposit account’.

Mafuru alieleza kuwa kutokana na uzoefu wake katika masuala ya kibenki, hakumbuki kama inawezekana mtu binafsi (mkuu wa taasisi) anaweza kupewa riba inayotokana na fedha za umma zilizowekwa kwenye akaunti hiyo maalum.

“Nimefanya kazi kwenye taasisi za benki karibu miaka 20 na nimekuwa nikipata wateja wanaofungua ‘fixed deposit account’ zikiwemo taasisi za umma huko nyumba. Sikumbuki, nasema sikumbuki namna yoyote ambayo inawezekana benki kumlipa mtu binafsi riba ya umma,” alisema.

“Nasema sikumbuki, sijawahi kuona na sijawahi kufanya hivyo,” alisisitiza.

Hata hivyo, Mafuru alieleza kuwa kutokana na tuhuma hizo zilizotolewa na Rais John Magufuli, mkutano wake na Kamati ya Hesabu za Serikali uliofanyika mjini Dodoma ulimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum ili kubaini kama kuna vitendo viovu vilivyofanywa na wakuu wa taasisi za umma.

Kauli hiyo ya Mafuru inakubaliana na kauli iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu ambaye alikuwa mmoja kati ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA. Profesa Ndulu alisema kuwa sio dhambi kuweka fedha kwenye akaunti hiyo.

Rais Magufuli atoboa siri ya kuteua wanajeshi Serikalini
Warioba: Maadili yameporomoka kwa viongozi na jamii