Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameiandikia Chadema barua nyingine baada ya kutoridhishwa na majibu ya barua aliyokiandikia chama hicho awali.

Jaji Mutungi amewapa chadema siku tano tangu Machi 2 hadi 6 mwaka huu kujibu hoja kwanini chama hicho kisichukuliwe hatua kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa kwa kufanya maandamano bila kibali na kutoa lugha za uchochezi.

“Nimesoma vyema barua yako, ila nasikitika kwamba barua yako haikujielekeza kujibu hoja ya msingi ambayo ilihitaji chama chako kitoe maelezo kuhusu uvunjifu wa kanuni za maadili ya vyama vya siasa na sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992, hususan kauli ya mwenyekiti wa chama chenu, Freeman Mbowe ambaye katika mkutano wa kamepni za chama chenu uliofanyika Mwananyamala kwa Kopa, Februari 16 alisikika akiongea maneno ya uchochezi,” inasomeka sehemu ya barua ya Msajili.

Msajili aliyanukuu maneno ya Mbowe ambayo alidai anaongoza mapambano na kwamba lazima wakubali kubeba majeneza ili kuleta haki.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kuwa watajibu barua hiyo ya Msajili leo, Jumatatu.

Chanzo cha barua hizo ni kitendo cha Chadema kufanya maandamano kutoka Mwananyamala kwenda Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao, Februari 16.

Katika maandamano hayo, askari wa jeshi la polisi alifyatua risasi ambayo ilisababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.

Video: Askofu Kakobe afunguka tena, Msajili aitisha tena Chadema
Ajali yaua watano na kujeruhi tisa