Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi jana aliitolea ufafanuzi kauli ya Rais John Magufuli kuhusu mwenendo wa shughuli za kisiasa nchini na kudai kuwa wanaoipinga wameitafsiri tofauti.

Jaji Mutungi amesema kuwa Rais Magufuli hakumaanisha kuzuia harakati za kisiasa nchini, bali kauli yake ililenga katika kuzuia siasa zisizo na tija na zilizolenga katika kukwamisha mipango ya maendeleo.

Alisema kuwa Rais alikuwa akiwataka wanasisa wenzake pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana naye katika kuleta maendeleo nchini na kuachana na siasa zisizo na tija.

“Rais alikuwa akijaribu kuwasihi wanasiasa kuangalia namna ya kujikita kwenye siasa ya maendeleo ya jamii kwa ujumla na kuachana na siasa za kupinga maendeleo,” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi alivitaka vyama vya siasa kutekeleza demokrasia kwa vitendo ndani ya vyama vyao na sio kuhubiri demokrasia nje ya chama huku wao hawaitekelezi.

Katika hatua nyingine, Jaji Mutungi alivitaka vyama vya siasa kuhakikisha vinawasilisha gharama za uchaguzi kwa muda huku akivitaja vyama vilivyowasilisha kwake gharama hizo hadi sasa kuwa ni ACT-Wazalendo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wanachi (CUF).

Alisema kuwa chama kisichowasilisha gharama za uchaguzi kwa muda kitakabiliwa na adhabu kisheria, na kwamba mgombea asiyewasilisha gharama hizo anaweza kufungwa jela kwa mwaka mmoja au faini ya shilingi milioni mbili au vyote kwa ujumla.

Rama Dee Adai ameolewa Australia, ajipanga kutoka na mdundo wa ‘Singeli’
Ukawa wawaka, wadai Serikali iandae Magereza za kutosha kuwafunga