Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa nchini akitoa onyo na kuwataka wale wote wanaotumia vibaya jina la ofisi ya Msajili ili kuichafua ofisi yake au kwa lengo la kukidhi hisia na matakwa yao binafsi waache kabisa tabia hiyo, Baraza la Udhamini la Chama cha Wananchi (CUF) limesema linafanya utaratibu wa kuzikutanisha pande mbili za uongozi wa chama hicho kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo.
“Tunauomba umma wa Watanzania kutambua kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni taasisi inayoendeshwa kwa kufuata misingi na taratibu za sheria za nchi. Aidha tunawaasa wadau wa habari kutoa taarifa baada ya kujiridhisha na usahihi wa taarifa hizo, na kujikita kwenye taarifa zinatolewa rasmi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa badala ya kuuaminisha umma na kuupotosha kwa makusudi,” ilieleza taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Monica Laurent wa Ofisi ya Msajili.

Kwa siku kadhaa sasa CUF imekumbwa na mgogoro wa kiuongozi kati ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wake aliyepata kujiuzulu na kurejea tena Profesa Ibrahim Lipumba.

Kwa upande wake, Baraza la Udhamini la CUF kupitia kwa Mwenyekiti wa kikao kilichoketi wiki hii na Mjumbe wa baraza hilo, Peter Malebo alisema mgogoro uliopo ndani ya chama hicho utamalizwa ndani ya chama hicho baada ya kuzikutanisha pande hizo mbili.

“Tatizo lililopo ndani la CUF ni tatizo la muda mrefu na wajumbe wa bodi ya chama hicho ndio wenye jukumu la kumaliza mgogoro huo, lakini mbaya zaidi baadi ya wajumbe wamekuwa ndio wanachonganisha na kukuza mgogoro huo badala ya kuumaliza,” alisema Malebo.

Aidha, Malebo alisema wanampongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa kutolea ufafanuzi wa sakata la uongozi wa chama hicho na kumthibitisha Profesa Lipumba kuwa ni Mwenyekiti halali wa chama hicho kwa mujibu wa chama chao.

 

 

Serengeti boys yawasili nchini kichwa chini
Watafiti nchini wagundua programu ya kuchunguza saratani ya kizazi kwa simu