Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amejibu tamko la Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) waliodai kuwa watamfungulia mashtaka endapo hatachukua hatua dhidi ya CCM ikiwa ni pamoja na kukifuta chama hicho kwa kuonesha ujumbe wa chuki na ubaguzi katika sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema kuwa hawezi kuwazuia Bavicha kumpeleka mahakamani kwani hiyo ni haki yao. Lakini akawashauri kuwa kabla hawajazungumza walichozungumza ni vyema kwanza wangemuuliza na kuwa na uhakika kwani tayari ameshachukua hatua za kisheria dhidi ya CCM.

“Wanatakiwa kuwa na uhakika kwanza,” alisema Jaji Mutungi. “Mimi nimeshawachukulia hatua CCM, tena hatua kwa mujibu wa sheria. Nimewaandikia barua nikiwataka wajieleze kuhusu ujumbe huo ulioonekana,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Jaji Mutungi alisema kuwa tayari ofisi yake imeshaingilia mgogoro wa uchaguzi unaoendelea visiwani Zanzibar kwa kuwa unawahusu wadau ambao ni vyama vya siasa. Alisema amezungumza na pande mbili zinazozana ili kusaidia katika kupata maridhiano ya amani.

Magwiji wa Dawa za Kulevya wanaswa na serikali ya Magufuli
Mtoto wa Kikwete ahusishwa Kuuziwa UDA kwa bei yaKutupwa, kukwepa kodi