Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili nchini Rwanda, Kizito Mihigo ameieleza mahakama kuwa ameachana na ombi lake la rufaa dhidi ya hukumu ya kifungo cha miaka 10 alichoanza kukitumikia tangu mwaka 2015 kwa kosa la uhaini.

Uamuzi wa Kizito umetolewa Jumatatu wiki hii baada ya Mahakama kumpa nafasi ya kuanza kujitetea kufuatia maombi yake ya rufaa aliyoyawasilisha miaka miwili iliyopita.

Kizito mwenye umri wa miaka 37 alikutwa na hatia ya kupanga njama za kutaka kumuua Rais Paul Kagame pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu nchini humo.

Alishtakiwa kwa kujihusisha na shughuli zilizolenga kuleta machafuko nchini humo. Pia, kushirikiana na kundi la upinzani ya Rwanda National Congress ambalo liko uhamishoni pamoja na kundi la waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo la FDLR.

Alihukumiwa kifungo hicho pamoja na mwandishi wa habari, Cassien Ntamuhanga, ambaye alihukumiwa miaka 25 jela lakini aliachiwa mwaka 2017; na mwanajeshi mstaafu Jean Paul Dukuzumuremyi ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Mwanasheria wa mwimbaji huyo, Antoinette Mukamusoni ameviambia vyombo vya habari kuwa mteja wake alifanya maamuzi ya kuachana na rufaa hiyo bila kushinikizwa.

“Aliiandikia barua mahakama Juni 26 na kunipa nakala ya barua hiyo. Ni kweli alisema hataki tena kuendelea na rufaa, hii ni haki yake na ni sahihi kama mteja mwenyewe anaona hataki kuendelea na rufaa,” alisema mwanasheria huyo.

Mwanamuziki huyo hakueleza sababu hasa zilizomfanya kuamua kutumikia kifungo cha miaka 10 na kuachana na rufaa hiyo.

George Weah aweka urais pembeni na kuwakabili Nigeria
Bashe asema anaweza kutimkia upinzani, ‘kama...’