Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD), imesema kuwa hali ya dawa kwa sasa ni nzuri na zinapatikana kuliko kipindi kingine chochote baada ya kuboresha mambo mbali mbali ikiwemo Serikali kutenga bajeti kubwa yenye kukidhi kasi ya uingizaji dawa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, amesema hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa imeboreshwa na kuimarika kutoka asilimia 54  hadi kufikia asilimia 74 na kuwahakikishia wananchi na umma kwa ujumla kuwa upatikanaji wa dawa utaimarika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu hadi kufikia asilimia 90.

Aidha, Bwanakunu amesema kuwa MSD imefanikiwa kurejesha Maghala iliyokuwa imekodi kwa ajili ya kuhifadhia vifaa tiba, hatua ambayo imeokoa sh.bilioni 4 ambazo zilikuwa zikilipwa kama kodi kila mwaka.

Hata hivyo ameongeza kuwa, ndani ya wiki ijayo wanatarajia kuzindua  duka la dawa la MSD Mkoani Katavi, ambapo watakuwa wamefikisha idadi ya maduka Saba, mengine yakiwa Mkoani Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Lindi, Geita na Mbeya.

Kwa sasa MSD inanunua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ,ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba una kuwa endelevu na kupunguza gharama za ununuzi wa dawa hizo ambazo asilimia 80 zinatoka nje ya nchi

Jaffo atoa onyo kwa waganga wakuu
Video: Mtatiro aibua madai ya wizi wa fedha CUF, ataja waliohusika