Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa amechambua uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumfukuza uanachama Bernard Membe, uamuzi uliofanywa jana, Februari 28, 2020.

Akizungumza na TBC1, Msekwa ameeleza kuwa uamuzi huo umefuata taratibu na kanuni za chama, hivyo unafaa kuitwa uamuzi wa chama.

“Mbele ya macho ya kanuni mwanachama ni mwanachama, anaweza kuwa kiongozi au asiwe kiongozi, lakini akishatuhumiwa utaratibu ni uleule,” alisema Msekwa.

Aliongeza kuwa uamuzi uliotolewa ni uamuzi unaomlenga mtuhumiwa na unapaswa kupokelewa na jamii kama yalivyotolewa hasa kama yametolewa kwa haki na kufuata kanuni.

“Narudia kusema haya ni maamuzi kama maamuzi yanayofanyika na mahakama, yanafuata taratibu na yakishatolewa hayaleti hofu yoyote katika jamii hata kama ni uamuzi wa kumnyonga mtu hauleti hofu yoyote,” aliongeza Mzee Msekwa.

Membe alifukuzwa uanachama ikiwa ni siku chache zimepita tangu alipohojiwa na Kamati ya chama hicho inayoshughulikia masuala ya nidhamu.

Membe anadaiwa kupanga njama ya kukikwamisha chama hicho katika mchakato wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Kamati Kuu ya CCM pia imempa karipio kali Katibu Mkuu wa zamani, Abdulrahman Kinana pamoja na adhabu ya kutogombea nafasi ya chama kwa kipindi cha miezi 18, lakini pia Katibu Mkuu wa zamani, Yusufu Makamba yeye amesamehewa.

Makampuni ya ulinzi yasiyosajiliwa kwenye mfumo wa PSGP kufungiwa
Magufuli ashiriki dua kuepusha Corona, kwenye msikiti mkubwa nchini