Simba imemshusha nchini mshambuliaji wa pili kutoka Senegal ndani ya wiki moja, Pape Abdoulaye N’daw baada ya Papa Niang aliyetua nchini Jumamosi na kucheza dhidi ya Mwadui ya Shinyanga kwa dakika 45 na kiwango chake kutowaridhisha wengi kutemwa rasmi.

Simba imekuwa ikihangaika kupata mshambuliaji aliyekamilika na hivyo kulazimika kuleta nchini wachezaji kadhaa, wakiwamo washambuliaji ili kutafuta mmoja atakayemaliza tatizo la ufungaji wa mabao linaloikabili.

Habari ambazo gazeti hili lilizipata jana kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo zilisema kuwa Niang alipewa mkono wa kwa heri juzi muda mfupi baada ya kutoridhisha benchi la ufundi.

“Kabla ya kuja nchini tulipewa sifa nyingi kuhusu Niang, lakini tumemwona sivyo tulivyoambiwa na watu wengi hawajamkubali, hivyo tumeona tuachane naye mapema kwani hatakuwa msaada.

“Sisi tunataka kutafuta mshambuliaji wa uhakika ambaye,atakuwa yuko vizuri katika upachikaji wa mabao, ambaye ataiwezesha timu yetu kufanya vizuri kwenye ligi,” alisema kiongozi huyo.

Niang amemuacha nyuma yake N’daw pia kutoka Senegal ambaye anatarajiwa kujaribiwa Jumamosi pamoja na mshambuliaji mwingine kutoka Mali.

Hata hivyo, N’daw alijikuta na wakati mgumu jana saa 3:30 asubuhi baada ya kutua nchini na kugandishwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa dakika 47 bila mwenyeji wake (uongozi wa Simba) kufika ili kumpokea.

Msenegali huyo, muda wote alikuwa akijaribu kufanya mawasiliano na uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya mapokezi kwa kuwa ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutua nchini. Akiwa uwanjani hapo, N’daw alisema, “Niko hapa kwa ajili ya mazoezi na Simba na ninamngoja kiongozi mmoja aje kunipokea ili niende kupumzika kwa ajili ya kuanza majaribio.”

Hata hivyo, hakutaka kuzungumza suala hilo, alisema,” Nimetoka Senegal nilikokuwa nikiichezea klabu ya Niary Tally, lakini awali nilikuwa nikiichezea Dynamo Bucurest ya Romania. Naamini ujio wangu utaifaidisha klabu, pia nitaiwezesha kutwaa ubingwa. “Nina umri mdogo wa miaka 20, nina uzoefu wa kutosha. Ninaweza kucheza ligi yoyote yenye ushindani, ikiwamo ile inayochezwa kwa kutumia nguvu. Nimecheza timu kubwa na sasa nimekuja kufanya kazi kwenye timu kubwa Tanzania, hivyo naamini nitafanya makubwa na kuisaidia Simba.

Mwonekano wake

N’daw ana urefu wa futi 6.5, sawa na sentimita 195. Ni mwembamba, mchangamfu na anaonekana kuwa na mwili kama ilivyo kwa wachezaji Michael Olunga wa Gor Mahia au beki Vincent Bossou wa Yanga.

Alisema,” Nikiwa Dynamo Bucuresti, msimu wa mwaka jana nilicheza michezo 11 kati ya 38 na kufunga mabao saba.

“Sikucheza michezo mingi kwa sababu nilikuwa majeruhi, lakini hata hivyo sikukata tamaa, baada ya kuihama hiyo timu na kurudi nyumbani (Senegal) na nimekuwa nikiichezea Niary Tally kwenye msimu wa mwaka huu na mpaka sasa nimecheza michezo minane na kufunga mabao matano.”

Kocha Kerr amsifu

Kocha wa Simba, Dylan Kerr alisema, “N’daw atamaliza tatizo la ufungaji, lakini ataisaidia Simba kwenye mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. “Naamini anaweza kumaliza matatizo yetu, awali tulikubaliana niwaletee mchezaji na N’daw ndiye mchezaji mwenyewe.”

Kupimwa kwa Mtibwa Jumamosi

Hata hivyo, Simba itampima mchezaji huyo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, wakati itakapocheza dhidi ya Mtibwa Sugar.

Misri Yajitoa All African Games 2015
Serena Williams Kumaliza 2015 Akiwa Kileleni?