Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amefunguka na kudai kuwa hawezi kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwani imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha uchumi wa nchi kutokana na kudai kwamba wananchi hawana pesa na wawekezaji wamekimbia tofauti na hali ilivyokuwa awamu nyingine zilizopita.

”Siwezi kuipongeza Serikali sababu imeporomosha uchumi, hakuna pesa kwenye mifuko ya wananchi, enzi za Mkapa na Kikwete uchumi ulikuwa unavuta wawekezaji lakini uchumi huu wawekezaji wanaonekana ni wezi wakwepa kodi” amesema Msigwa.

Mchungaji Msigwa amesema kuwa uchumi wa nchi unaanguka kutokana na mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali ya awamu ya Tano, ametaja mambo hayo kuwa ni makusanyo yote ya Serikali za mitaa yanaenda Serikali kuu lakini pia amezungumzia suala la Serikali kuanzisha miradi mikubwa inayotumia gharama kubwa bila hata kusihirikisha na kupitishwa na Bunge huku kipato cha nchi kuwa chini zaidi hali inayopelekea serikali kukopa madeni makubwa.

Amemtaka Waziri wa Fedha, Dkt Philip Mpango aeleze ni uchumi wa aina gani anaouamini huku akidai kwamba baadhi ya mambo anayoyafanya sasa ni tofauti na alivyokuwa akifanya enzi za uongozi wa Rais Kikwete.

Hivyo amewataka wabunge kutokuwa wanafiki kwa kusifia uchumi wa nchi kukua huku wananchi na wabunge wenyewe hawana pesa na kudai uchumi mtaani ni mbovu, amewataka wabunge kutuumia nafasi yao bungeni vizuri kujadili mambo ambayo ni kero kwa wananchi bila kujali itikadi za vyama.

Hayo ameyaongea bungeni  pindi akichangia hoja katika mjadala wa Bajeti kuu ya Serikali 2018/2019.

P - Funk awapa nondo wasanii wa Bongo Fleva, ‘usikurupuke’
Serikali yafaidika bilioni 1.5 gawio la TTCL