Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amemkosoa vikali Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kuwa anakandamiza na kuwanyanyasa wabunge wa upinzani.

Msigwa amesema kuwa Ndugai anaongozwa na Serikali hivyo hawezi kufanya chochote kinyume na maagizo yanayotoka Serikalini hivyo nguvu kubwa ameielekeza kuukandamiza upinzani.

“Tunachomlaumu Ndugai ni kwamba ametekwa na Serikali kiasi kwamba Bunge la Tanzania limegeuka kuwa mhuri, kwa hiyo Bunge kuwepo pale ni kumaliza hela za wananchi kwa sababu hakuna mahali ambapo linaikosoa Serikali, meno pekee ambayo bunge linayo ni kuwatoa wabunge wa upinzani ndani ya Bunge,”amesema Msigwa.

Akijibu hoja hiyo, Spika Ndugai amesema kuwa hayo ni mawazo yake tu na kwamba mbunge huyo ni miongoni mwa viongozi wa Bunge, hivyo kama kuna mapungufu basi na yeye ni sehemu yake.

Hata hivyo, Msigwa ameongeza kuwa kwa sasa wanapita katika kipinndi ambacho Serikali haifuati sheria ipasavyo, pamoja na kufanya kazi nzuri ya ukusanyaji mapato, haiwezi kutumia fedha hizo bila Bunge kuidhinisha.

 

Polisi: Lissu hatoki Ng'o, mpaka upelelezi ukamilike
LIVE: Rais Magufuli akizindua mradi wa maji Uvinza Kigoma