Sababu ya wachezaji wa Klabu Bingwa Tanzania Bara kushindwa kupanda gari la wazi lililokua limendaliwa maalum na uongozi wa klabu hiyo, kwa lengo la kutembeza kombe la ubingwa, imefahamika.

Uongozi wa Simba uliandaa gari la wazi na tayari lilikua limeshafika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya shughuli maalum, lakini zoezi hilo lilishindikana na wachezaji walipanda basi dogo (Mini Bus Coaster).  

Sababu ya zoezi hilo kukwama inatajwa kusababishwa na kocha mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Bara mara tatu mfululizo Sven Vandenbroeck kugomea wachezaji wake kupanda gari la wazi.

Kocha Sven ndiye aliyeanza kutoka nje ya uwanja huo na kuelekea upande yalipokuwa yamepaki magari ya mashabiki na gari maalum ambalo liliandaliwa kuwabeba wachezaji.

Kisha baada ya dakika moja akarudi tena ndani lakini wakati akiwa mlangoni akaonekana kuanza kuzozana na mwanadada Lispa Hatibu ambaye ni msaidizi wa ofisa Mtendaji mkuu wa Simba Senzo Mazingisa.

Mabishano hayo yalidumu kwa dakika moja kabla ya wahudumu wa uwanja na kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola kuwasihi waache ndipo Lispa alipoamua kuondoka kwa hasira huku akifoka.

Inadaiwa chanzo cha mzozo huo ni Sven kugoma wachezaji kupanda gari la wazi ambalo lilipangwa kupita katika barabara mbalimbali za Dar es Salaam mpaka makao makuu ya klabu hiyo Msimbazi huku yeye akitaka timu kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa nusu fainali ya Kombe La Shirikisho dhidi ya Young Africans utakayofanyika Jumapili.

Hata hivyo kocha Sven ni kama alishinda vita hiyo kwani alikomaa na msimamo wake wa kutoruhusu wachezaji kupanda gari la wazi hivyo wachezaji kupanda basi dogo (Mini Bus Coaster).

Prof. Makubi: Kutoa huduma za afya za uhakika ni jukumu letu
Stones kujihukumu mbele ya bosi