Msimamo uliowekwa wazi na Rais John Magufuli kuhusu mchakato wa katiba mpya umempa wakati mgumu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika mahojiano na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita, Rais Magufuli alisema kuwa mchakato wa Katiba mpya sio kipaumbele kwenye utawala wake na akataka aachwe ainyooshe nchi kwanza.

Lissu amepinga vikali msimamo huo wa Mkuu wa Nchi akisisitiza kuwa Katiba mpya ni muhimu kuliko kubadili vipengele vya katiba iliyopo.

“Tulishaondoka kwenye mjadala wa kuziba viraka kwenye Katiba, tumeshakubaliana kwamba tunahitaji mabadiliko ya Katiba yote si sehemu tu. Rais asidhani mtu akikalia kiti hicho basi neno lake ni sheria ya nchi. Haiwezekani,” anakaririwa.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, alisisitiza kuwa nchi inapaswa kuanza mchakato wa katiba mpya kwa kuiangalia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na sio hatua iliyofikiwa na Bunge la Katiba.

“Kama Rais Magufuli anataka kunyoosha nchi, anapaswa kuirejea Rasimu ya Jaji Warioba. Tuanzie hapo, zaidi ya hivyo atajidanganya na kuwadanganya Watanzania,” alisema.

Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva alisema kuwa Ofisi yake itaitolea ufafanuzi hivi karibuni kwani ni jukumu lake.

TB Joshua atabiri mshindi wa Urais wa Marekani na majanga yatakayomkuta
Al Masry Wachafua Hali Ya Hewa Zamalek SC