Mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Brenda Maro amesema kuwa msongo wa mawazo kupitiliza unaweza kupelekea mtu kuwa na kitambi.

Amebainisha  hayo katika mahojiano na Mtanzania, na kueleza kuwa hali hiyo inatokana na homoni aina ya Cortisol zijulikanazo kama hormonal stress ambazo zinazalishwa mara baada ya mtu kupata msongo wa mawazo kupitiliza.

” stress hormone (cortisol) ikitolewa kwa wingi inachangia au inachochea uhifadhi wa mafuta mwilini, hasa kwa wale wanawake ambao tayari wana maumbo makubwa ya tumboni” amesema daktari Maro.

Ameeleza kuwa homoni hizo za Cortisol zinapozalishwa huwa zinakawaida ya kujikusanya sehemu za tumbo na kusababisha uhifadhi wa mafuta katika eneo hilo.

” Aina hiyo ya homoni zina tabia ya ‘ku – realocate’ sehemu za tumbo, inatagemea lakini sio kila mwanamke au mwanaume anapata. lakini kulingana na utafiti, aina hiyo ya homoni inachochea uhifadhi wa mafuta” ameongeza daktari Maro.

Licha ya kuwa inategemea mtu ana kiwango gani cha stress, lakini kadri inavyozidi ndivyo uzalishaji wa homoni hizo unavyozidi pia.

Hata hivyo amebainisha kuwa hali hii ya vitambi vya stress inawakumba zaidi wanawake kuliko wanaume.

Lakini amebainisha kuwa sababu nyingine ya wanawake kuwa na vitambi ni baada ya mwanamke anapofikia kikomo cha uzazi kwani hupelekea kuwa na ‘location’ kubwa ya mafuta tumboni.

” Kuna homoni inaitwa oestrogen, hizi huwa zinachochea mafuta sehemu za hips, lakini mwanamke anapofikia kikomo cha uzazi homoni hizo zinazalishwa kwa kiasi kidogo hivyo kwa wanawake wengi inasababisha mafuta kuhifadhiwa tumboni” alifafanua daktari Maro.

Aidha ametoa ushauri kwa watu kujiweka katika hali au mazingira ambayo yanaweza kupunguza msongo wa mawazo na pia kuzingatia aina ya vyakula ambavyo haviongezi mafuta mwilini ili kusaidia kupunguza uwezekano wa kupata vitambi.

 

Manuel Neuer kustaafu soka 2020
Kocha timu ya taifa afukuzwa kambini baada ya kubeti