Mshambuliaji kutoka nchini Chile Alexis Sanchez, amesema yupo katika wakati mgumu wa kukabiliana na changamoto za msongo wa mawazo, kuhusu maisha ya jijini London.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amesaliwa na muda wa miezi 18 katika mkataba wake wa sasa, na tayari ameshatamanishwa na ofa ya mshahara wa Pauni 400,000 kwa juma kutoka kwenye moja ta klabu zinazoshiriki ligi kuu ya soka nchini China.

Hata hivyo mshambuliaji huyo ambaye tayari ameshaifungia Arsenal mabao 14 katika michezo 23 aliyocheza msimu huu, anaendelea na mazungumzo ya kusaini mkataba mpya wa kuitumikia The Gunners.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari nchini England zinaeleza kuwa, Sanchez ameutaka uongozi wa Arsenal kumuongezea mshahara kutoka Pauni 130,000 hadi 250,000 kwa juma.

Ombi hilo bado linafanyiwa kazi na viongozi wa Arsenal ambao walikuwa tayari kumuongezea mshahara wa Pauni 180,000 katika mkataba mpya ambao upo mezani kwa sasa.

Akizungumza na jarida la klabu (Club Magazine), Sanchez alisema maisha ya London yamekua rafiki kwake lakini suala lililo mbele yake kwa sasa linamchanganya na kuanza kuhisi huenda maisha hayo yakaharibika.

Alisema mara zote amekua anaona maisha ya London yana tofauti kubwa na mahala pengine ambapo aliwahi kuishi, na wakati mwingi amekua akiutumia muda wake kukaa nyumbani na kufanya mambo yake binafsi.

“Ninapendezwa na maisha ya London, kuhusu vyakula vinywaji na ukaribu wa rafiki zangu,” Alisema Sanchez

“Ninatamani kuendelea kukaa hapa, lakini suala linalonikabili kwa sasa kuhusu mustakabali wa maisha ya baadae kuhusu soka langu linanichanganya, na sina budi kufanya maamuzi ya haraka. Aliongeza mshambuliaji huyo.

Sanchez alijiunga na Arsenal mwaka 2014 akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 31.7.

Mpaka sasa ameshaitumikia The Gunners katika michezo 82 na kufunga mabao 41.

Steve Holland Athibitishwa The Three Lions
Polisi Makao Makuu watoa tamko kuhusu kupotea kwa Msaidizi wa Mbowe